Nasari wa NDC ahaha kujinasua kwenye Uhujumu Uchumi

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Gideon Nasari, bado anapambana kuchomoka katika shauri la rushwa, kutakatisha fedha na matumizi mabaya ya madaraka wakati akiwa ofisini.

Shauri hilo ni moja ya mashauri mengine mawili yanayoendelea kuchunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika ofisi zake za Dar es Salaam.

Nasari ameongoza NDC kuanzia 2007 hadi 2014.

Sambamba na Nasari, katika shauri hilo pia yumo aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja. Nado hawajafikishwa mahakamani. Ngeleja ana tuhuma hizohizo za Nasari katika mradi wa chuma na  makaa ya mawe, Liganga na Mchuchuma.

Taarifa zilizotufikia zinaeleza kwamba Nasari, kama Ngeleja, wamegundulika kuwa na utajiri mkubwa wa mali ambao unatia shaka.

Pamoja na Nasari, Ngeleja kuwasilisha vielelezo na maelezo kuhusu utajiri wao, bado Serikali kupitia TAKUKURU, haijaridhika hivyo kuwataka kuwasilisha mengi zaidi juu ya halali wa vigogo hao kumiliki mali zaidi ya vipato vyao halali.

Miongoni mwa mali hizo ni Nasari kuwa na nyumba tano jijini Dar es Salaam na nyingine Arusha, huku Ngeleja akielezwa kuwa na nyumba tatu za kifahari, kiwanda cha kuzalisha pombe kali na mali zingine zenye thamani kubwa, yakiwamo magari.

Taarifa zinaeleza kwamba baada ya uchunguzi kukamilika, wawili hawa wanaweza kufikishwa mahakamani.