Magufuli afyeka vigogo 13 waliotia nia ubunge 2020

Watendaji wa serikali 13  walioandika barua za kuomba likizo bila malipo ili wapate nafasi ya kugombea ubunge, wamefutwa kazi jumla.

Vigogo hao wamo Wakuu wa Wilaya, Mkoa, Wakurugenzi wa Mashirika na Taasisi za Umma, ambao ni wateule wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu Katiba.

Habari zinaeleza kuwa watendaji hao, hata baada ya kumsikiliza Rais John Magufuli akisema hapendi kuona wateule wake wakiingiwa tamaa ya ubunge na kuamua kuacha kazi, lakini wao waliamua kujaribu.

Taarifa kutoka chanzo chetu zinaeleza kuwa Rais Magufuli anawaona vigogo hao kuwa na kiburi, hivyo kuchukua hatua ya kuwafuta kazi moja kwa moja. Inaelezwa kuwa Rais amekasirishwa kutokana na watendaji hao kukaidi kile kinachoelezwa kuwa maono yake katika uongozi.

Tayari Rais Magufuli amejaza baadhi ya nafasi za vigogo hao kwa kuteua wengine.

“Kuna watu hadi Leo hawajaelewa staili ya uongozi ya Magufuli, hawa ndiyo wanaokumbwa na matatizo, huyu Msukuma hataki kujaribiwa,” kilidokeza chanzo kimoja cha taarifa hii.

Ikulu imekuwa ikitoa taarifa za kuteuliwa kwa viongozi wapya wa nafasi mbalimbali zilizoachwa na vigogo hao ambao tunaweza kusema ‘wametumbuliwa.’ 

Baadhi ya vigogo hao nafasi zao zinaonekana kujazwa, lakini taarifa hazielezi endapo watapangiwa kazi nyingine au vinginevyo. Wapo pia wanaoelezwa kuwa wamestaafu au kupangiwa kazi nyingine.

Wengine zaidi kutemwa kesho

Kesho, Jumatatu, Julai 6, 2020 Rais Magufuli anatarajiwa kutangaza kujaza nafasi za baadhi ya mashirika ya umma na taasisi kwa vigogo walioandika barua za kuacha nafasi zao ili wakagombee ubunge.

Tanzania haina sheria inayozuia watendaji wake kutangaza nia ya kugombea ubunge, lakini uamuzi binafsi wa Rais Magufuli umetisha wengi kuomba uteuzi wa vyama vyao ili kuwakilisha wananchi bungeni.