Magufuli agoma kuwabariki baadhi ya vigogo wa serikali walioandika barua kuomba wakagombee ubunge

Pamoja na kusema hadharani kwamba atawaruhusu wale waliomwandikia barua, lakini ukweli ni kwamba hakupenda wateule wake “waingie tamaa ya kutaka ubunge.”

Wiki moja iliyopita tuliandika tukidokeza kwamba vigogo 13 walioandika barua kwa Katibu Mkuu Kiongozi wakiomba likizo bila malipo ili kutangaza kutia nia ya kuwania ubunge kupitia CCM watafyekwa.

Baada ya habari hiyo baadhi ya vigogo hao walionekana Dodoma wakihaha “kuzichomoa” barua zao kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi au Ikulu kabla hazijamfikia Rais Magufuli.

Katika harakati hizo za kuchomoa barua hizo, wengi wamekwama na sasa hawana la kufanya isipokuwa kusubiri utashi wa Rais Magufuli.

Miongoni mwa vigogo walioshindwa kufanikisha kuchomoa barua zao ni Godfrey Mwambe, aliyekuwa Mkurugezi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji (TIC).

Tangu wiki iliyopita, tarehe 4 Julai, Mwambe aliyeonekana Dodoma akihaha kutoka ofisi moja hadi nyingine ili kufanikisha azma yake ya kutengua uamuzi wake – kwa kuchomoa barua, sasa nafasi yake imetangazwa na Rais Magufuli kwamba inajazwa na Dk. Maduhu Kazi.

Uchunguzi wetu umebaini kuwa Mwambe anakwenda kugombea ubunge wa Jimbo la Masasi.

Hata hivyo, tunazo taarifa kwamba Mwambe hatachaguliwa kuwania ubunge huo katika mchakato wa wilaya na hata kama atapenya, vikao vya juu vya vya uteuzi CCM vinavyoongozwa na Rais Magufuli havitapitisha jina lake.